Kamati Tendaji ya “Project ECHO” Tanzania, iliyo chini ya Wizara ya Afya, imekutana Dodoma leo katika kikao chake cha 12 cha mwaka kilichofanyika katika Hoteli ya Morena na kuwakutanisha wadau mbalimbali katika Sekta ya Afya wakiwemo wataalamu kutoka TAMISEMI, Wizara ya Afya, Wataalamu wa Maabara, wadau wa maendeleo katika sekta ya afya na wataalam kutoka mabaraza ya wataam (Professional councils), Chuo kikuu Mzumbe na wafadhili wa Mradi (CDC).

Kikao hicho kilifunguliwa na Mwenyekiti wa muda wa Kikao hicho Bi. Mary Mtui, Msajili wa Baraza la Wataalamu wa Maabara kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Serikali.  Amesema, pamoja na mambo mengine kikao hicho, kimekusudia kujadili na kuweka mikakati ya namna ya kuongeza ushiriki wa wataalamu wa Afya katika mafunzo kwa njia ya mtandao “ECHO Platforms” pamoja na namna wataalamu wa afya wanavyoweza kupanda madaraja/vyeo kwa kushiriki kwenye mafunzo hayo ambayo yanatolewa kila wiki kupitia vituo 9 (hubs) na watoa huduma za afya kutoka katika vituo (Spokes) zaidi ya 349 vilivyofungiwa vifaa vya mafunzo nchi nzima wananufaika na mafunzo hayo.

Miongoni mwa mafunzo yanayotolewa kwa sasa ni pamoja na kliniki za “Adult HIV, Pediatric HIV, MDR TB, HVL, HIV LAB, Supply Chain na AMS/IPC ECHO”. Hadi kikao cha 12 cha mwaka cha Kamati ya Utendaji, inakadiriwa zaidi ya CPD pointi 1000 zimetolewa kwa watumishi wa afya ambao wamekuwa wakipata mafunzo kwa njia hiyo ya mtandao, huku zaidi ya watumishi na watoa huduma za afya 650 wakishiriki mafunzo nchini nzima kila wiki.

Kikao hicho kimeweka mikakati mingi ya kuendelea kuwajengea uwezo watumishi wa afya popote walipo kwa kupata mafunzo ya kina yatakayosaidia kuboresha huduma za afya katika vituo vyote vya Afya nchini, pamoja na kuongeza wigo wa mafunzo kwa kutumia vifaa vya kisasa kwa kushirikiana na wafadhili, ili uwekezaji huo uweze kuwa na tija katika utoaji huduma za afya kwa wananchi.

Wakichangia mkutano huo, wadau wamepongeza Serikali kupitia Wizara ya Afya na Wadau wa maendeleo CDC kwa kuwekeza katika mfumo wa mafunzo kwa njia ya mtandao; na hivyo kuwajengea uwezo wataalamu wa Afya wakiwa mahali pa kazi.

Akieleza mikakati zaidi ya Wizara; Mratibu wa Project ECHO Tanzania Bw. Jacob Lusekelo amesema, Wizara inakusudia kupanua wigo wa mafunzo na usimamizi kwa kuanzisha “Super Hub” nchini ambayo itakuwa na uwanda mpana zaidi wa kutoa mafunzo, mwongozo na usimamizi kwa wataalamu wa huduma za afya (immersion training).

Kikao hicho cha siku moja kimehudhuriwa na mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Serikali, Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulikia Huduma za Afya (TAMISEMI), pamoja na viongozi wengine kutoka Wizara ya Afya, TAMISEMI, wawakilishi kutoka Mabaraza ya Kitaaluma Tanzania, Chuo Kikuu Mzumbe, MDH, THPS, MNH na NBTS.

 

Mkurugenzi Msaidizi wa Afya TAMISEMI, Dkt. Paul Chaote, akikabidhi kitabu cha mwongozo wa utekelezaji wa shughuli za mradi wa

ECHO Tanzania “ECHO Framework” kwa Mwenyekiti wa kikao Bi. Mary Mtui  (Msajili wa Baraza la Wataalamu wa Maabara) kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Serikali.

Mwenyekiti Bi. Mary Mtui (wa kwanza kushoto), akiendesha kikao cha Kamati Tendaji ya Project ECHO Tanzania, Dodoma.

Katikati ni Mratibu wa Project ECHO Tanzania Bw. Jacob Lusekelo, ambaye pia ni katibu wa Kamati hiyo.

Kulia ni Dkt. Miraji Ally Chaih, Mshauri Mwandamizi wa Mradi wa ECHO kupitia CDC -  Mzumbe.

Baadhi ya wajumbe wa mkutano wa Kamati Tendaji ya Project ECHO Tanzania, wakifuatilia  majadiliano wakati wa kikao.

Wajumbe wa Mkutano wa Kamati Tendaji ya Project ECHO Tanzania, wakiwa katika picha ya Pamoja baada ya kuhitimisha kikao.

Walioketi katikati ni Mwenyekiti wa kikao Bi. Mary Mtui, kulia kwako ni Dkt. Mackfallen Anasel wa Chuo Kikuu Mzumbe na kushoto kwake ni Dkt. Paul Chaote, kutoka TAMISEMI.

 

 

News and Updates

Mzumbe University,
P.O Box 1 Mzumbe,
Morogoro, Tanzania.
Tel: 255 (0) 23 2931220/1/2
Fax: 255 (0) 23 2931216
Cell: 255 (0) 754694029
Email: .
Go to top