Vijana Wasomi nchini Tanzania wametakiwa kuwa wabunifu na kutumia usomi wao kutatua tatizo la ajira kwa kuacha kufikiria zaidi kuajiriwa na Serikali au na makampuni makubwa na badala yake watumie fursa zinazowazunguka zikiwemo kilimo,viwanda na biashara ili kuweza kujiajiri na kujiatia kipato.

 

Hayo yamesemwa na Waziri wa ofisi ya Makamu wa Rais (mazingira na Muungano) Mh. Januari Makamba amewataka vijana na wasomi  wakati akifungua kongamano la majadiliano na kubadilishana fikra kwa vijana wasomi wa chuo kikuu mzumbe lililoandaliwa na jukwaa la vijana ‘Think Tank’ kwa lengo la kutambua fursa, mitaji na masoko.

 Alisema kuwa Serikali haiwezi kuajiri wasomi wanaohitimu kwenye vyuo vyote hapa nchini hivyo kuelekea uchumi wa viwanda vijana wasomi wanayo fursa ya kufanya shughuli mbalimbali za kujipatia  kipato kupitia sekta ya viwanda.

 Akitoa mada katika kongamano hilo Mkurugenzi wa vipindi na uendeshaji wa Clouds Media group, Ruge Mutahaba alisema kuwa wakati huu wa ulimwengu wa sayansi na teknojia lazima vijana wabadilishe fikra za kusubiri kuajiriwa na badala yake watafute maarifa ya kujiajiri.

 Mutahaba alisema kuwa katika kuelekea uchumi wa viwanda vijana wanayo nafasi nzuri ya kupiga hatua ya maendeleo kupitia sekta ya viwanda, kilimo, ufugaji, uvuvi na shughuli nyingine za ujasiliamali.

 Naye mratibu wa jukwaa la vijana Think Tank Suma Mwaitenda alisema kuwa jukwaa hilo linakusanya mawazo ya vijana ambao wamejitolea kuleta fikra mpya kwa ajili ya kuleta maelendeo.

 Alisema kuwa kila mwaka vijana wanaohitimu vyuo  mbalimbali hapa nchini ni  takribani 800,000 hadi 1,000,000 hata hivyo wanaopata ajira Serikalini na sekta binafsi ni asilimia 10 pekee, hivyo makongamano hayo yatasaidia kubadilisha fikra na kuwapa maarifa vijana ya kujiajiri na hatimaye kuisaidia serikali kutatua changamoto ya ajira na kukuza uchumi.

 Alivitaja vyuo watakavyofanya kongamano kama hilo kuwa ni pamoja na chuo cha tiba Muhimbili, Udom, Mtakatifu Agustino, shule ya sheria na Chuo Kikuu Dar es Salaam.

 Kwa upande wake mwanafunzi wa chuo hicho Asha Sungura alisema kuwa kongamano hilo limeweza kumsaidia kuongeza maarifa na ubunifu katika ujasiriamali wa kilimo cha zabibu anachofanya mkoani Dodoma.

 Alisema kuwa kongamano hilo limemsaidia kufahamu namna ya kuongeza thamani ya bidhaa anayozalisha pamoja na kutafuta mitaji na masoko hivyo aliwashauri wanafunzi wenzake kutokata tamaa na mitaji waliyonayo badala yake waanze na mitaji midogo ambayo itaongezeka.

 

 

News and Updates

Mzumbe University,
P.O Box 1 Mzumbe,
Morogoro, Tanzania.
Tel: 255 (0) 23 2931220/1/2
Fax: 255 (0) 23 2931216
Cell: 255 (0) 754694029
Email: .
Go to top