Chuo Kikuu Mzumbe ni miongoni mwa taasisi zinazoshiriki katika Kongamano la tatu la Kitaifa la wiki Ufuatiliaji, Tathmini na Kujifunza. Kongamano hilo linafanyika kwa muda wa siku nne kuanzia tarehe 17 - 20 Septemba 2024 katika ukumbi wa Golden Tulip Airport Hotel, Zanzibar Tanzania likibebwa na kaulimbiu isemayo; “Kuboresha utoaji wa huduma kwa kutumia teknolojia katika ufuatiliaji na tathmini,”.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kongamano hilo, Mgeni Rasmi ambaye ni Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa niaba ya Rais wa Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar, Mhe.
 
Hemed Suleiman Abdulla amezitaka taasisi kutumia fursa ya kongamano hilo ili kupata maarifa yatakayozisaidia taasisi hizo pamoja na serikali katika shughuli za maendeleo. Aidha Mhe. Abdulla amesisitiza kuwa Ufuatiliaji, Tathmini na kujifunza ndio nyenzo muhimu katika msingi wa mafanikio yoyote yale katika jamii.
Chuo Kikuu Mzumbe kinashiriki Kongamano hilo kikiwa ni Sehemu ya wadhamini na wadau wakubwa wa taaluma ya Ufuatiliaji, Tathmini na Kujifunza ambayo inatolewa Chuoni kwa ngazi ya Shahada ya Awali pamoja na Shahada ya Umahiri.
 
Vilevile Chuo Kikuu Mzumbe kimetoa wahadhiri ambao wanashiriki moja kwa moja katika kongamano hilo wakiwemo wanakamati wa maandalizi, wanajopo wa mijadala ya kitaaluma na kitaalamu pamoja na mtoa mada elekezi ambaye ni Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. William Mwegoha.
 
Kongamano hilo linaloratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu kwa kushirikiana na Tume ya Mipango ya Zanzibar Chini ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar linalenga kutoa fursa kwa wadau wote, ikiwemo serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali, sekta binafsi, na washirika wa maendeleo, kushirikiana kikamilifu katika kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji na tathmini pamoja na kukuza uwazi na uwajibikaji katika utekelezaji wa sera na miradi ya maendeleo, kwa kuleta pamoja wadau mbalimbambali.
******************************** 
 
Mzumbe University,
P.O Box 1 Mzumbe,
Morogoro, Tanzania.
Tel: 255 (0) 23 2931220/1/2
Fax: 255 (0) 23 2931216
Cell: 255 (0) 754694029
Email: cmu@mu.ac.tz
Go to top