Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof. William Mwegoha amesema Mzumbe iko tayari kushirikiana na wadau wengine wa ndani na nje ya nchi katika kubadilishana uzoefu katika maeneo ya taaluma na tafiti.

Prof. Mwegoha amesema hayo leo Agosti 14, 2024 wakati wa hafla ya kusaini hati ya makubaliano kati ya Chuo Kikuu Mzumbe na Chuo Kikuu cha Bonn yanalolenga kuimarisha uhusiano wa kitaaluma na kuboresha ubora wa elimu, utafiti na ubunifu baina ya vyuo hivyo.

Awali, Prof. Detlef Mueller-Mahn kutoka Chuo Kikuu cha Bonn amesema ni fursa kwao kuimarisha ushirikiano utakaoleta tija baina vyuo hivyo kwa kuinua viwango vya elimu ya juu na utafiti katika nyanja mbalimbali huku ukihimiza uvumbuzi na ubunifu.

Makubaliano hayo ya ushirikiano yanaelekeza ushiriki wa Chuo Kikuu Mzumbe katika miradi ya utafiti na kuboresha mitaala ili kukidhi mahitaji ya soko ya ajira kimataifa. Pia, ushirikiano huo utaleta fursa za semina, warsha na kongamano za kitaaluma zinazolenga kujadili changamoto na mbinu bora za kuboresha elimu na utafiti.

Hati ya makubaliano baina ya Chuo Kikuu Mzumbe na Chuo cha Bonn ni ya miaka mitano kufuatia kukamilika kwa awamu ya kwanza ambapo wanataaluma wamenufaika na fursa za masomo na tafiti katika nyanja za taaluma na tafiti.

*****

 

 

Mzumbe University,
P.O Box 1 Mzumbe,
Morogoro, Tanzania.
Tel: 255 (0) 23 2931220/1/2
Fax: 255 (0) 23 2931216
Cell: 255 (0) 754694029
Email: cmu@mu.ac.tz
Go to top