Wanachama wa Chama Cha Wafanyakazi (THTU) Chuo Kikuu Mzumbe wametakiwa kuzingatia na kuzielewa sheria mbalimbali zinazowaongoza na kuwalinda kama wafanyakazi kwa kusoma miongozo ya kazi ili waweze kuimarisha uwajibikaji na ufanisi kazini.
Hayo yamebainishwa Aprili 5, 2024, katika Mkutano Mkuu wa Mwaka wa viongozi na wanachama wa Chama Cha Wafanyakazi (THTU) Chuo Kikuu Mzumbe uliofanyika kwa kuzingatia matakwa ya Katiba ya Chama hicho.
 
Akizungumza katika Mkutano huo, Mwenyekiti THTU Taifa Dkt. Paul Loisulie amewataka wanachama kuzingatia mambo ya msingi yanayohusu maslahi na haki za wafanyakazi ikiwemo kuwajibika kwa masuala yao mbalimbali ya kawaida ambayo yapo chini ya uwezo wao badala ya kila jambo kuwapelekea viongozi.
 
Awali, akifungua mkutano huo, Mwenyekiti wa Chama Cha wafanyakazi Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt. Adria Fuluge amewataka wajumbe kuhamasishana ili watu wengi wajiunge na THTU kutokana manufaa ya chama hicho sambamba na kuzielewa sheria mbalimbali zinazowaongoza na kuwalinda kama wafanyakazi.
Katibu mkuu wa Chama Cha wafanyakazi (THTU) Chuo Kikuu Mzumbe Dkt. Bahati Ilembo amesema ni muhimu kuzingatia yale yote yanayojadiliwa kwa maslahi ya wafanyakazi ili kuimarisha mahusiano bora kazini.
 
Aidha Mhasibu wa Chama hicho Bw. Godfrey Mujuni aliwasilisha kwa wajumbe mapato na matumizi kwa mwaka 2023 na makadirio ya bajeti ya mwaka 2024 ili kutoa nafasi ya kuipitisha kabla haijapelekwa kwenye kamati kuu Taifa.
Sambamba na hilo, Wajumbe wa mkutano huo walipata elimu iliyotolewa na tabibu kutoka Kituo cha Afya Chuo Kikuu, Dkt. Athumani Mwananyemla ambaye alielezea kuhusu ugonjwa wa ini kwa kufafanua chanzo cha ugonjwa huo, dalili zake, chanjo yake na njia za kujikinga na ugonjwa huo.
Mkutano huo ulihudhuriwa na wajumbe mbalimbali wa chama hicho kutoka Kampasi kuu Morogoro, Ndaki ya Mbeya na Ndaki ya Dar es Salaam.
 

 

Mzumbe University,
P.O Box 1 Mzumbe,
Morogoro, Tanzania.
Tel: 255 (0) 23 2931220/1/2
Fax: 255 (0) 23 2931216
Cell: 255 (0) 754694029
Email: .
Go to top