Chuo Kikuu Mzumbe katika kuadhimisha Siku ya Wanawake duniani leo Machi 6, 2024 kimetoa msaada kwa waathirika wa mafuriko katika Wilaya ya Kilosa wenye thamani ya Shilingi 4,135,000/-

Akiwasilisha msaada huo, Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Allen Mushi amesema Mzumbe ina utamaduni wa kugusa jamii kila Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambapo kwa mwaka huu msaada uliotolewa umekuwa mahususi kwa kaya zilizokumbwa na mafuriko hapa wilayani Kilosa.

“Tumeleta sare za shule kwa watoto wa kike na kiume, madaftari, kalamu na penseli, miswaki na dawa za meno. Vifaa vingine ni pamoja na sabuni za kufulia, taulo za kike na chumvi.” Prof. Mushi aliweka bayana.

Aidha, amesema kuwa kwa muda wa siku tatu Chuo Kikuu Mzumbe kupitia Kituo cha Msaada wa Kisheria kutoka Kitivo cha Sheria kimeendelea kutoa huduma za kisheria bure katika masuala ya mirathi, ardhi, ndoa na masuala mtambuka wilayani hapo ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.

Akipokea misaada hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mhe. Shaka Hamdu Shaka ameushukuru uongozi na timu ya wawakilishi kutoka Chuo Kikuu Mzumbe kwa msaada huo na kusisitiza kuwa Wilaya hiyo imekumbwa na mafuriko makubwa toka mwezi Desemba 2023.

“Ninakuhakikishieni kwamba msaada huu utawafikia walengwa na tunakupongezeni sana kwa kutoa msaada wa kisheria kwa siku tatu wilayani kwetu, mwitikio ni mkubwa na ninashauri tuweke utaratibu endelevu wa kusogeza huduma hii kwa wananchi walau huduma hii iwe inatolewa kila mwezi” Amesisitiza Mhe. Shaka.

Amesema Chuo Kikuu Mzumbe kimechagua mahali sahihi kutoa huduma ya kisheria kwa kuwa Kilosa ni wilaya yenye migogoro mingi ya ardhi, ndoa na mirathi; hivyo, msaada huo ni vema ukawa endelevu ili kutatua changamoto zinazowakabili wakazi wa wilaya hiyo.

Haya yote yanafanyika ili kuiishi kaulimbiu ya Chuo Kikuu Mzumbe: "Tujifunze kwa maendeleo ya watu"

*****

 

 

Mzumbe University,
P.O Box 1 Mzumbe,
Morogoro, Tanzania.
Tel: 255 (0) 23 2931220/1/2
Fax: 255 (0) 23 2931216
Cell: 255 (0) 754694029
Email: .
Go to top