Chuo Kikuu Mzumbe kupitia mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya kiuchumi ‘HEET’ kimeandaa warsha maalumu ya kuwajengea uwezo wanataaluma wake wanaofundisha masomo ya Teknolojia, Biashara,ubunifu na ujasiriamali kwa lengo la kulinda ubunifu ikiwa ni utekelezaji wa mradi wa HEET katika eneo la kujenga uwezo wa kufanya tafiti na ubunifu.
 
Akifungua warsha hiyo inayoendeshwa na Wataalamu kutoka Tume ya Sayansi na Teknolojia ‘ COSTECH’, Naibu Mratibu wa mradi wa HEET Chuo Kikuu Mzumbe Dkt.Hawa Tundui amesema kuwa pamoja na malengo mengine, mradi wa HEET umekusudia kuviwezesha vyuo vikuu nchini kufanya tafiti zitakazoleta tija zaidi kwa jamii na kutatua changamoto pamoja na kuwawezesha Wanataaluma kuandaa miradi ya kiubunifu na kuhakikisha ubunifu huo unasajiliwa na kulindwa na hivyo chuo kimeandaa warsha hiyo ili Wanataaluma na wanafunzi waweze kunufaika na ubunifu wao.
 
Akiwasilisha mada kwenye warsha hiyo mtaalamu kutoka COSTECH Dkt. Georges Shemdoe amesema kuwa Hataza ‘Patent’ ni haki ya kisheria anayopewa mbunifu ya kukataza mtu mwingine asitengeneze, asitumie na asiuze ubunifu huo bila idhini yake na kwamba ni tofauti na haki miliki na hivyo ni muhimu kusajili wazo la kibunifu katika hatua za mwanzo kabisa ili apate haki ya kunadi ubunifu wake wa kipekee bila kuwa na hofu ya kuigwa.
 
Katika hatua nyingine kaimu Meneja wa kitengo cha ubunifu, ujasiriamali na ushirikiano wa viwanda wa Chuo Kikuu Mzumbe Dkt.Emmanuel Chao amesema kuwa mafunzo hayo yatachochea zaidi ubunifu wa Wanafunzi na Wanataaluma wa chuo kikuu Mzumbe kwani kupitia kituo cha ulezi wa ubunifu na ujasiriamali anachokisimamia (Entrepreneurship & Innovation incubation centre) wamekuwa wakipokea na kulea mawazo mengi ya kibunifu kutoka kwa Wanafunzi na Wanataaluma na sasa kituo hicho kitawaongoza wabunifu hao katika mchakato mzima wa kupata haki na hati miliki za mawazo yao ili kuyalinda kisheria.
 
Nae Mwanafunzi wa kitivo cha Sayansi cha Chuo Kikuu Mzumbe Frank Msonge ameshukuru chuo kikuu Mzumbe kuweza kuwapatia mafunzo hayo na kusema kuwa hayo ni mafunzo muhimu sana kwani Wanafunzi wengi hutumia akili kwenye ubunifu ikiwa ni sehemu ya masomo yao na hivyo wakiwezeshwa kuyalinda itawasaidia kuyaendeleza na kuchangia kuongeza chachu ya maendeleo ya teknolojia nchini.
*******************
 
 
 
 

 

Mzumbe University,
P.O Box 1 Mzumbe,
Morogoro, Tanzania.
Tel: 255 (0) 23 2931220/1/2
Fax: 255 (0) 23 2931216
Cell: 255 (0) 754694029
Email: .
Go to top