Chuo Kikuu Mzumbe kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi kwa Tanzania, “Higher Education for Economic Transformation” (HEET) kimewakutanisha wadau kutoka taasisi mbalimbali ili kupokea maoni na ushauri kwa ajili ya programu mpya ya Shahada ya Umahiri katika Sayansi za Fedha za Kigitali , yaani “Master of Science in Digital Finance” inayotarajiwa kuanzishwa na Chuo hicho.
 
Akizungumza wakati wa kikao hicho leo Februari 5, 2024 katika Ndaki ya Dar es Salaam, Mhadhiri wa Kitivo cha Sayansi na Teknolojia, Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt. Morice Daudi amesema kikao hicho kimelenga kupokea maoni na ushauri kutoka kwa wadau wa nje ili kuboresha mtaala wa programu hiyo ambayo inaunganisha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano na huduma za kifedha.
Dkt. Daudi amesema kuwa utoaji wa huduma za kifedha kupitia njia za kidijitali umeongezeka, ikiwemo malipo tunayofanya kwa njia ya simu “mobile money”, miamala ya kibenki, utoaji wa mikopo, bima, na mitaji.
 
Ameongeza kuwa programu hiyo itatoa wahitimu mwenye weledi utakaowawezesha kujiari na kuajiriwa katika eneo la huduma za kifedha za kidijitali.
Dkt. Daudi amefafanua kwamba pamoja na mambo mengine, wahitimu watakuwa na uwezo wa kuchambua data zinazokusanywa katika eneo la fedha ili kupata uelewa mpana wa kiuwekezaji, viashiria hatarishi na mwelekeo wa masoko unaotokana na mwenendo wa kifedha.
 
Aidha, Dkt. Daudi ameongeza kuwa ni matarajio ya Chuo Kikuu Mzumbe ni kuona mwanafunzi atakayehitimu katika Shahada hiyo anatumia maarifa atakayokuwa amejifunza ili kuweza kufanya ubunifu katika eneo la fedha. Vilevile, inatarajiwa kwamba mhitimu huyo aweze kuunda mifumo mbalimbali ya ki-TEHAMA itakayowezesha huduma za kifedha kuendelea kuwa bora.
“Tunawashukuru sana wadau ambao wametupatia maoni, ushauri na kuboresha kile tulichonacho kwani nchi hii tunaijenga kwa pamoja na ili kuweza kupata maoni vizuri lazima kushirikisha wadau wa nje ili watujuze ni kitu gani tuboreshe ili kuifanya hii programu kuwa shindani na yenye ubora unaohitajika” Alisema Dkt. Daudi.
Naye mmoja wa washiriki wa kikao hicho kutoka Benki ya NMB, Bw. Paul Shilla ameupongeza uongozi wa Chuo Kikuu Mzumbe kwa mchakato wa kuanzisha digrii ambayo ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi. Ameongeza kuwa teknolojia inakua na kuleta mabadiliko katika huduma za fedha; hivyo, wanafunzi wanatakiwa kupatiwa ujuzi sahihi kwenye masuala ya fedha kulingana na mazingira yanavyobadilika.
Kikao hicho ni miongoni wa utekelezaji wa shughuli zinazofadhiliwa na Mradi wa HEET katika eneo la pili linalohusu kuboresha Mtaala na Kuanzisha Mbinu za Kibunifu za Ufundishaji (Upgrading Curriculum and Introducing Innovative Pedagogical Methodologies), na kimeshirikisha wadau kutoka taasisi mbalimbali zikiwemo Benki ya NMB, Tume ya TEHAMA, Skuli ya Biashara ya Chuo Kikuu Dar es Salaam, Bodi ya Wahasibu (NBAA), na Soko la Hisa la Dar es Salaam (Dar es Salaam Stock Exchange).
                                                                 ********
 
 
 
 
 
 
Mzumbe University,
P.O Box 1 Mzumbe,
Morogoro, Tanzania.
Tel: 255 (0) 23 2931220/1/2
Fax: 255 (0) 23 2931216
Cell: 255 (0) 754694029
Email: .
Go to top