Katika kuhitimisha semina elekezi kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza Chuo Kikuu Mzumbe, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Mipango, Fedha na Utawala, Prof. Allen Mushi amezungumza na wanafunzi hao kwa niaba ya Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. William Mwegoha.
Akizungumza na wanafunzi hao tarehe 01 Novemba 2023, katika ukumbi wa Samora Chuo Kikuu Mzumbe Kampasi Kuu Morogoro, Prof. Mushi amewapongeza wanafunzi hao kwa kufanikiwa kujiunga na Chuo Kikuu Mzumbe na amewahakikishia kuwa wapo mahali sahihi na salama kwa wakati sahihi, kwani historia ya Chuo hicho na watu waliowahi kusoma Chuoni hapo inatosha kuthibitisha ubora na umahiri wake.
“Mzumbe imekuwa sehemu ya kuandaa viongozi, wajasiriamali na wataalamu wanaoisaidia jamii na Taifa katika nyanja mbalimbali. Tunawakaribisha nanyi pia ili kuwa sehemu ya wataalamu hao hapo baadaye”. Alisema Prof. Mushi.
Aidha, Prof. Mushi amewaelekeza wanafunzi hao kuhusu muundo wa uongozi na mgawanyo wa majukumu wa Chuo Kikuu Mzumbe kuanzia kwa Mkuu wa Chuo mpaka Serikali ya Wanafunzi na amewataka kuendelea kufuatilia ili kufahamu wapi watatakiwa kwenda pindi watakapohitaji kupata msaada wa kitaaluma au kijamii kwa kipindi chote watakachokuwa masomoni.
Awali akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina hiyo, Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Taaluma, Tafiti na Ushauri wa Kitaalamu, Dkt. Eliza Mwakasangula, aliwasisitiza wanafunzi hao kuzingatia lengo namba moja ambalo limewaleta Chuo Kikuu Mzumbe, ambalo ni taaluma/kusoma. Dkt. Eliza amesema siri ya mafanikio ni maadili na kujituma.
“Ninatamani kuona mnafanikiwa katika taaluma, na siri kubwa katika kufanikisha hilo ni kuzingatia maadili na kujituma”. Alisema Dkt. Eliza.
Wanafunzi pia walipata wasaa wa kuuliza maswali na kutoa maoni yao kwa ajili ya kuboresha mazingira yao ili kuhakikisha wanafanikiwa.
 
Karibu Chuo Kikuu Mzumbe, “Tujifunze kwa Maendeleo ya Watu”
 
Kwa picha zaidi za Tukio hili,Tembelea ukurasa wetu wa Facebook,Bofya Hapa
 
Mzumbe University,
P.O Box 1 Mzumbe,
Morogoro, Tanzania.
Tel: 255 (0) 23 2931220/1/2
Fax: 255 (0) 23 2931216
Cell: 255 (0) 754694029
Email: .
Go to top