Matokeo ya utafiti wa haki za watu waishio na Virusi vya UKIMWI (WAVIU) Tanzania uliofanywa na Chuo Kikuu Mzumbe umeonyesha kupungua kwa kiasi kikubwa unyanyapaa kwa watu wanaoishi na virusi, huku elimu kubwa ikihitajika kwa wananchi kuelea haki za WAVIU.

 Hayo yameelezwa leo wakati wa warsha ya wadau iliyoandaliwa na Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu Mzumbe, wakati wa kuwasilisha matokeo ya Utafiti uliofanyika kwa mikoa ya Dar, Njombe, Shinyanga na Kilimanjaro.

 Akizundua Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof.William Mwegoha,amewapongeza na kuwashukuru wadau wote walioshiriki katika utafiti huo hususani Wafadhili Serikali ya Ubelgiji kupitia mradi wa VLIROUS unaotekelezwa na Chuo Kikuu cha Ghent kilichopo nchini Ubelgiji. na kusema kuwa uwasilishaji wa matokeo ya utafiti huo kwa Wadau ni jambo la msingi na unaleta maana zaidi kwa jamii kwani utawasaidia watu wengi kuelewa haki za watu wanao ishi na Virusi vya UKIMWI, pamoja na kuwawezesha wahusika kuchukua hatua pale wanapotendewa kinyume. 

 Kwa upande wake Mratibu wa huo kutoka Chuo Kikuu cha Ghent, Prof.Yves Jorens, amesema mradi huo wa ushirikiano kati ya Chuo Kikuu Mzumbe na Ghent, ulianza mwaka 2019 na kutakiwa kukamilika 2021 lakini ilishindikana kutokana na janga la UVIKO -19, hata hivyo wanafurahi unakwenda kukamilika ukiwa umeleta matokeo chanya na jamii itaendelea kuelimika kupitia njia tofauti ikiwemo programu tumizi (application) ya simu na filamu yenye kaulimbiu ya “TAMKA” iliyolenga kuwahamasisha watu kujitokeza na kuweka wazi hali zao kwa kuwa wanalindwa na Sheria.

 Awali akimkaribisha Makamu Mkuu wa Chuo, Mtiva wa Kitivo cha Sheria wa Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt.Seraphina Bakta,  alieleza kuwa utafiti huo ni maalum kwa ajili ya kulinda haki za binadamu, kwani kila mtu ana haki ya kuishi bila kubaguliwa ili aweze kufurahia haki nyinginezo za kibinadamu na kuishukuru Serikali, Wadau na Jamii kwa ushirikiano mkubwa iliyotoa wakati wote wa utafiti, uliopelekea mafanikio makubwa ya utafiti huo.

 Naye Mratibu wa utafiti huo ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt. Khanifa Massawe, alieleza kuwa matokeo ya utafiti huo yamejikita katika maeneo matatu ambayo ni kuwawezesha WAVIU kutambua haki zao, kuondoa unyanyapaa na kuongeza uelewa wa haki za WAVIU kwa jamii na WAVIU wenyewe. Kwa sasa Kitivo cha Sheria kinaendelea na jitihada za kuhusisha wadau muhimu katika kuhakikisha matokeo ya utafiti huo yanafanyiwa kazi na kuhusisha makundi yote msingi katika kuhakikisha uelewa wa haki za WAVIU unaongezeka pamoja na kuendelea kupunguza unyapaa binafsi.

 Warsha ya uwasilishaji wa matokeo ya utafiti huo imefanyika Makao makuu Morogoro mapema leo, na kuwashirikisha Wadau mbalimbali wakiwemo Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS), Baraza la Taifa la Watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI Tanzania (NACOPHA), Umoja wa watu waishio na virusi (HACOCA), Asasi za Kiraia zinazojihusisha na mapambano ya VVU, Maofisa Maendeleo na Ustawi wa Jamii, Viongozi wa dini, Taasisi za Utetezi wa Kisheria na Mawakili, Viongozi wa Kata ya Mzumbe, Wanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe na Wananchi.

*******************************************************************************************************

Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof.William Mwegoha, akizindua ripoti ya matokeo ya utafiti wa haki za watu waishio na Virusi vya

UKIMWI (WAVIU) Tanzania.

Mratibu wa mradi wa utafiti wa haki za watu waishio na Virusi vya UKIMWI (WAVIU) kutoka Chuo kikuu cha Genth, Prof. Yves Jores,

akizungumza katika Warsha hiyo.

Mkuu wa kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt.Seraphina Bakta akizungumza kuhusu umuhimu wa tafiti katika uwasilishaji wa ripoti ya

matokeo ya utafiti wa haki za watu waishio na Virusi vya UKIMWI (WAVIU).

Mratibu wa utafiti kutoka Chuo Kikuu Mzumbe ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu Mzumbe Dkt. Khanifa Massawe, akizungumza kuhusu umuhimu

wa mradi huo katika jamii.

Wadau mbalimbali walioshiriki katika uwasilishaji wa ripoti ya matokeo ya utafiti wa haki za watu waishio na Virusi vya UKIMWI (WAVIU)

Tanzania uliofanyika Chuo Kikuu Mzumbe, Kampasi Kuu, Morogoro katika picha ya pamoja.

News and Updates

Mzumbe University,
P.O Box 1 Mzumbe,
Morogoro, Tanzania.
Tel: 255 (0) 23 2931220/1/2
Fax: 255 (0) 23 2931216
Cell: 255 (0) 754694029
Email: cmu@mu.ac.tz
Go to top