Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha, ameongoza uzinduzi wa Baraza Jipya la Wafanyakazi, hafla iliyoangazia umuhimu wa mshikamano na ushirikiano kati ya uongozi na wafanyakazi wa chuo hicho.
Uzinduzi huo umefanyika tarehe 11 Desemba 2024, katika Ukumbi wa ICE, Chuo Kikuu cha Sokoine, Morogoro.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Prof. Mwegoha amesema, "Baraza hili ni msingi wa mafanikio yetu ya pamoja. Linatoa fursa kwa kila mfanyakazi kushirikisha mawazo yake kwa maendeleo ya taasisi na ustawi wa jamii ya Mzumbe.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na wajumbe 69, wakiwemo wawakilishi wa vitengo mbalimbali vya chuo, vyama vya wafanyakazi kama RAAWU na THTU, pamoja na wajumbe wa Menejimenti ya Chuo Kikuu Mzumbe.
Uzinduzi huo ulitanguliwa na uchaguzi wa wajumbe wa baraza, uliofanyika tarehe 10 Desemba 2024 katika Ukumbi wa Samora, Mzumbe. Baraza hilo linatarajiwa kuwa jukwaa muhimu la majadiliano ya masuala ya wafanyakazi na maendeleo ya chuo.
Aidha, Bi. Tulia Msemwa, Afisa Elimu Kazi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu Kamishna wa Kazi, alipongeza hatua ya kuanzishwa kwa baraza hilo na kusema, "Baraza hili litasaidia kuboresha mazingira ya kazi na kuhakikisha changamoto zinatatuliwa kwa haraka. Ni jukwaa muhimu la kuimarisha mahusiano kazini."
Vilevile, Ndg. Elia Kasalile, Katibu wa THTU Taifa, aliwapongeza wajumbe waliochaguliwa na kuwataka kusikiliza changamoto za wafanyakazi na kushirikiana na uongozi kuzitatua. "Nyie ni sauti ya wafanyakazi, hakikisheni masuala yao yanasikilizwa na kupewa kipaumbele," alisema.
Baraza hilo linatarajiwa kuwa nyenzo muhimu ya kuimarisha mshikamano, mawasiliano, na utendaji kazi bora ndani ya taasisi hasa katika wakati huu ambapo Chuo Kikuu Mzumbe kinatekeleza miradi mikubwa ya kuboresha miundombinu na huduma zake, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa kuongeza ubora wa elimu, tafiti, na ushirikiano wa jamii.