Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof.William Mwegoha, amesema kuwa chuo hicho kimejipanga kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia kwa kuendeleza na kuanzisha miradi ya maendeleo kwenye Kampasi zake zote tatu lengo ni  kutatua changamoto za miundombinu zinazokikabili chuo hicho.

Hayo ameyasema katika mkutano wake na Wanafunzi wa chuo hicho Kampasi Kuu, akihitimisha ziara kama hiyo aliyoifanya kwa Ndaki ya Mbeya na Dae es Salaam mwishoni mwa mwaka 2022. Mkutano huo ulilenga kutoa taarifa, kujadili changamoto mbalimbali za wanafunzi na kuweka mikakati ya pamoja katika kufikia malengo hususani katika masuala yanayowahusu moja kwa moja wanafunzi.

Amefafanua kuwa chuo kupitia mapato yake ya ndani kimetenga fedha kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa miundombinu ya kufundishia na kujifunzia ikiwemo uimarishaji wa mifumo ya TEHAMA, majengo ya Taaluma, mabweni, barabara za ndani, maji na kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa kujenga jengo la upasuaji katika kituo cha afya Kampasi kuu Morogoro utakaokwenda kwa pamoja na upanuzi wa zahanati ya Kampasi ya Mbeya.

Aidha ameongeza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Elimu imeanza utekelezaji wa mradi mkubwa  wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Uchumi (HEET) unaotekelezwa na vyuo vyote vya Umma mzumbe miongoni. Amesema kupitia mradi huo chuo kinategemea kujenga majengo  mapya na ya kisasa ya Taaluma, Maabara, kuboresha miundombinu ya Tehama, kuongezea ujuzi kwa wana taaluma pamoja na kuboresha mitaala itakayoendana na  soko la ajira la ndani na nje ya nchi, na kwamba mradi huo utakapokamilika utatatua changamoto nyingi zilizopo sasa.

Nao Wanafunzi hao wakizungumza kwa nyakati tofauti wameipongeza Menejimenti ya Chuo hicho kwa kuweka utaratibu wa kujadiliana na Wanafunzi masuala muhimu yahusuyo mustakabali wao chuoni hapo na kusisitiza kuwa utatuzi wa changamoto mbalimbali utasaidia kuboresha mazingira yao ya usomaji na kuendelea kukifanya Chuo Kikuu Mzumbe kuendelea kuwa chuo bora nchini Tanzania na barani Afrika kwa ujumla.

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na wajumbe wa Menejimenti ya Chuo ambao kwa nafasi mbalimbali walijibu hoja nakupokea changamoto na maoni ya wanafunzi katika kuendelea kuboresha ufundishaji.

******************************************************

Kaimu Makamu Mkuu wa chuo kikuu Mzumbe Prof.William Mwegoha akihitisha mjadala kwenye mkutano huo.

Kushoto kwake ni Naibu Makamu Mkuu wa chuo kikuu Mzumbe anayeshughulikia Mipango,Fedha na Utawala Prof.Allen Mushi.

Mkurugenzi wa Ustawi wa Wanafunzi wa Chuo kikuu Mzumbe Bi.Mariam Mattao akijibu hoja za Wanafunzi.

Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe anayeshughulikia Taaluma Dkt.Eliza Mwakasangula akijibu hoja zilizoibuliwa

na Wanafunzi kwenye mkutano huo.

Baadhi ya Wanafunzi wa masomo na ngazi mbalimbali wakitoa michango yao kuhusu utatuzi wa changamoto wanazokabiliana

nazo chuoni hapo.

 

Rais wa Wanafunzi wa Chuo hicho Bi.Akila Mollel akitoa shukrani kwa Menejimenti kwa niaba ya Wanachuo wenzake.

Mzumbe University,
P.O Box 1 Mzumbe,
Morogoro, Tanzania.
Tel: 255 (0) 23 2931220/1/2
Fax: 255 (0) 23 2931216
Cell: 255 (0) 754694029
Email: mu@mzumbe.ac.tz
Go to top