Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu Mzumbe Prof. Saida Yahya Othmani ametangaza kupambana vikali dhidi ya unyanyasaji wa kingono kwa yeyote atakayehusishwa na tuhuma hizo katika kipindi chake cha uongozi Chuo Kikuu Mzumbe.
Prof. Saida ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na Menejimenti ya Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam katika kikao kilichofanyika kwenye kituo cha Tegeta.
Ameeleza kuwa unyanyasaji wa kingono (Sexual harassment) haukubaliki katika mazingira yeyote na hivyo kuwataka Wanawake kwa Wanaume wa jumuiya ya chuo hicho kuwa huru kuripoti matukio yote yanayoashiria jambo hilo, naye atalivalia njuga kuhakikisha hatua stahiki zinachukuliwa kwa mhusika bila kujali wadhifa wake.
 
“Hatutofumbia macho ukatili wa kingono kwa fununu zozote zitakazomhusu yeyote wakati wowote,watu wote wawe huru kuripoti matukio.” Alisisitiza Prof.Saida
Katika hatua nyingine Mwenyekiti huyo ameipongeza Menejimenti ya Chuo hicho kwa jitihada zake hususani katika ujenzi wa miundombinu na uendelezaji wa Taaluma.
Amesema ametembelea Kampasi zote tatu na kujionea jitihada za Menejimenti hiyo kwenye utendaji makini unaozingatia weledi na ufanisi na kuahidi kuendeleza jitihada hizo kwa ushirikiano wa pamoja katika masuala yote hususani zaidi kwenye eneo la utafiti ambalo ndiyo msingi wa taaluma na hutumika kama kigezo muhimu katika kukipa hadhi ya juu chuo kikuu chochote duniani.
Awali akimkaribisha kuzungumza na Menejimenti hiyo, Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof.William Mwegoha, alimpongeza Mwenyekiti kwa ziara zake na kueleza kwamba ziara hizo zimekuwa na manufaa makubwa kwa chuo kwani kupitia mikutano na Wafanyakazi baadhi ya changamoto za kisera zimekuwa zikipatiwa ufumbuzi kwa majadiliano hayo ya pamoja
Mzumbe University,
P.O Box 1 Mzumbe,
Morogoro, Tanzania.
Tel: 255 (0) 23 2931220/1/2
Fax: 255 (0) 23 2931216
Cell: 255 (0) 754694029
Email: mu@mzumbe.ac.tz
Go to top