Watumishi wa sekta ya afya walio katika mafunzo ya Epidemiolijia kwenye mikoa ya Shinyanga na Tabora wamepongeza Chuo Kikuu Mzumbe kupitia mradi wa ‘CDC’ kwa kufadhili mafunzo hayo yanayoratibiwa na Wizara ya Afya yaliyolenga kuwajengea uwezo katika kukabiliana na magonjwa ya mlipuko,kufanya tafiti na uchakataji wa taarifa za afya.

Akizungumza na Timu ya ufuatiliaji wa mafunzo hayo wilayani Kishapu Mkoa wa Shinyanga, Dkt.Raymond Tibakya ambaye ni Mganga katika hospitali ya Wilaya ya Kishapu ya Dkt.Jakaya Kikwete, amesema  mafunzo hayo yamemsaidia kufahamu kwa undani kuhusu mifumo ya ufuatiliaji wa magonjwa, hatua iliyomwezesha kufanya uchunguzi kuhusu mfumo wa ufuatiliaji wa afya kwa Wakinamama wanaoishi na Virusi vya UKIMWI,kubaini mapungufu na kutoa mapendekezo kuhusu mfumo huo pamoja na kufanya utafiti kuhusu ongezeko la Virusi vya UKIMWI katika damu kwa Wagonjwa wanaoendelea na matumizi ya dawa za kufubaza virusi.

Aidha Dkt Tibyaka ameongeza kuwa kupitia mafunzo hayo aliweza kujumuika kwenye timu iliyoundwa kukabiliana na ugonjwa wa Kipindupindu uliotokea katika wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma na kufanikiwa kuutokomeza kupitia ujuzi alioupata katika mafunzo hayo na kushukuru chuo kikuu Mzumbe kwa kufadhili mafunzo hayo kupitia mradi wa CDC.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti mkoani Tabora Watumishi wa Hospitali Teule ya wilaya ya Sikonge Dkt.Neema Wilson na Bw. Laurent Lushekya ambaye ni Afisa Afya wa wilaya hiyo wamewapongeza waratibu na kusema kuwa mafunzo hayo ni muhimu sana kwani hadi sasa yamewasaidia kuboresha utendaji wao wa kazi tofauti na hapo awali na kuahidi kuutumia ujuzi huo kutatua changamoto za afya wilayani humo ambapo pia wameshukuru chuo kikuu Mzumbe na CDC kwa kuwawezesha kupata  mafunzo hayo.

Kwa upande wake Mhadhiri Mwandamizi na Mtaalamu wa kitengo cha Rasilimaliwatu katika mradi wa CDC wa Chuo Kikuu Mzumbe Dkt.Laurencia Mushi, amesema lengo kuu la mafunzo hayo ni kuisaidia Serikali kuimarisha mifumo ya afya nchini kwa kuwaongezea ujuzi Watumishi wa afya kupitia vyuo vya Umma na kuongeza kuwa hadi sasa Watumishi 15 wamehitimu mafunzo hayo katika awamu ya kwanza na 15 wengine wanaendelea na mafunzo  na kwamba program hiyo ni ya miaka mitano kuanzia mwaka  2021 hadi 2025.

Mzumbe University,
P.O Box 1 Mzumbe,
Morogoro, Tanzania.
Tel: 255 (0) 23 2931220/1/2
Fax: 255 (0) 23 2931216
Cell: 255 (0) 754694029
Email: .
Go to top