Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. Lughano Kusiluka amewataka Wanafunzi na Wanajumuiya wote wa chuo Kikuu Mzumbe kuienzi na kushiriki katika michezo mbalimbali inayoandaliwa chuoni hapo kwani michezo ni muhimu sana kwa afya zao kwa kuwa huwaepusha na magonjwa.

 Prof. Kusiluka amesema hayo katika sherehe za ufunguzi wa mashindano ya vitivo (Inter-faculty Games 2022) yaliyofanyika mwishoni mwa wiki katika viwanja vya michezo vilivyopo kampasi kuu Morogoro ambapo pia ameahidi kuboresha miundombinu ya michezo ikiwa ni pamoja na kununua vifaa mbalimbali vya michezo.

 “Menejimenti ya Chuo ina maono ya muda mrefu kuhusu michezo  kwa kuwa ni fursa kubwa ya kujitangaza na pia ni muhimu  kwa ajili ya afya zetu, pia tutambue kuwa michezo ni ajira na utajiri, kwahiyo tuendelee kuienzi michezo ”.Alisisitiza. 

 Katika hatua nyingine Makamu Mkuu wa Chuo amewapongeza Wanamichezo wote walioshiriki katika michezo ya TUSA mkoani Dodoma na kufanikiwa  kutwaa medali nyingi na kusema kuwa ana imani mwaka huu Wawakilishi hao wataleta medali nyingi zaidi.

 Ufunguzi wa mashindano hayo ambayo hufanyika kila mwaka ulihusisha michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, mpira wa pete, (Volleyball) na mpira wa kikapu na kuhudhuriwa na Wadau wa michezo wakiwemo Wafanyakazi wa Chuo Kikuu Mzumbe, Wanafunzi kutoka vitivo na skuli mbalimbali, Serikali ya wanafunzi na Wanajumuiya wengineo wa chuo kikuu Mzumbe.

            *********************************************************************************************

          Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof. Lughano Kusiluka akihutubia Wanamichezo waliohudhuria katika sherehe za mashindano ya vitivo 2022.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof. Lughano Kusiluka akipokea zawadi ya fulana za michezo kutoka kwa serikali ya Wanafunzi (MUSO)

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof. Lughano Kusiluka, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe (Taaluma) kushoto Prof. William Mwegoha, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe (Utawala na Fedha) Prof. Allen Mushi  na kushoto kwa Prof. Mwegoha ni bi. Akila Molle Rais wa Serikali ya Wanafunzi  (MUSO).Kulia kwa Makamu Mkuu wa Chuo ni viongozi wengine wa MUSO na Wanafunzi wakifuatilia Mtanange wa mechi kati ya Kitivo cha Sheria na Skuli ya biashara

Timu za mpira wa pete zikiwa katika mashindano ya vitivo.

Timu mbalimbali za Wanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe wakimskiliza Makamu Mkuu wa Chuo

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof. Lughano Kusiluka akiwapa mkono Wachezaji wa Timu ya mpira wa miguu kutoka kitivo cha Sayansi na Teknolojia

 

Viongozi wa Chuo Kikuu Mzumbe pamoja na Viongozi wa Serikali ya Wanafunzi wakiwa katika picha ya pamoja na Wachezeshaji (Referees) wa mpira wa Miguu

 

Mzumbe University,
P.O Box 1 Mzumbe,
Morogoro, Tanzania.
Tel: 255 (0) 23 2931220/1/2
Fax: 255 (0) 23 2931216
Cell: 255 (0) 754694029
Email: .
Go to top