Katika kuunga mkono jitihada za Serikali za kupambana na uharibifu wa mazingira unaosababisha athari kubwa za Mabadiliko ya Tabia Nchi, Chuo Kikuu Mzumbe kimeanza kampeni ya upandaji Miti; ikiwa ni sehemu ya kutekeleza Sera yake ya Mazingira.

 Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Lughano Kusiluka ameongoza mamia ya wanafunzi kutoka Kitivo cha Sayansi na Teknolojia (FST) kupanda miti zaidi ya 1000 kwenye eneo la Barabara kuu kuingia Chuo Kikuu Mzumbe Kampasi Kuu eneo la Maekano Kata ya Mzumbe Wilaya ya Mvomero.

 Akizungumza mara baada ya kushiriki zoezi hilo; Makamu Mkuu wa Chuo alishukuru ushirikiano mkubwa wa wanafunzi kushiriki zoezi hilo; na kwamba kitendo hicho kitabaki kuwa historia katika Maisha yao kwakuwa watakuwa wameacha alama isiyofutika.

 “Ushiriki wenu umeacha kumbukumbu ya kesho kwakuwa hata mtakapomaliza shule mtakumbuka miti ambayo mmeipanda na kuancha alama. Huu ni moyo wa kizalendo na ambao mnapashwa kuwarithisha wengine kujali na kulinda mazingira ili kuondokana na athari kubwa za mabadiliko ya tabia nchi yanayochangiwa kwa kiasi kikubwa na uharibifu wa mazingira” Alisema

 Aidha ameahidi Chuo Kikuu Mzumbe kuendelea kuwa mabalozi wema katika kampeni ya upandaji miti, na kwamba tayari kama chuo wana sera ya Mazingira inayotoa dira ya kutunza mazingira na kuunga mkono jitihada za Serikali katika kulinda mazingira.

 Mkuu wa Kitivo cha Sayansi na Teknolojia wa Chuo Kikuu Mzumbe Dr. Joseph Sungau amesema waliamua kuanza na kampeni ya kupanda miti kama sehemu ya elimu kwa wanafunzi kwa kutambua kazi kubwa ya miti kisayansi katika kupambana na madhara yatokanayo hewa chafu inayozalishwa na shughuli za kibinadamu vikiwemo viwanda, magari na mitambo mbalimbali na kwamba kwa kupanda miti kwa kiasi kikubwa kinapunguza athari za uwepo wa hewa chafu.

 “Tumeanza na miti hii michache lakini lengo letu ni kuendelea kuwafundisha wanafunzi wetu sayansi kwa vitendo kwa kuanza na masuala haya ya upandaji miti ambayo yanafaida za moja kwa jamii.

 Zoezi hilo ambalo lilifanyika kwa kushirikisha Chuo Jirani SUA kupitia wakala wa kimataifa wa mazingira “Earth Day Network” limekuwa chachu kwa jamii inayozunguka Chuo Kikuu Mzumbe kwa kuona umuhimu wa kuendelea kuhamasisha na kutoa elimu kwa jamii kuhusu faida za upandaji miti.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof. Lughano Kusiluka akishiriki kampeni ya upandaji miti eneo la Maekani Kata ya Mzumbe, Morogoro.

 

Mkuu wa Kitivo cha Sayansi na Teknolojia Dr. Joseph Sungau akipanda mti wakati wa kampeni ya kupanda miti iliyofanywa na Chuo Kikuu Mzumbe. Akishuhudia pembeni ni Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Lughano Kusiluka, na baadhi ya wanafunzi mwaka wa kwanza wa Kitivo cha Sayansi na Teknolojia.

Mwakilishi wa wakala wa kimataifa wa mazingira “Earth Day Network”  kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA) Bi. Zuhura Ahmed akiwakilisha jumuiya hiyo kwenye shughuli ya upandaji miti iliyofanyika Maekani  Mzumbe– Morogoro. Jumuiya hiyo inahusisha wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali vya mkoani Morogoro.

Vijana wanachuo wa Chuo Kikuu Mzumbe walioshiriki zoezi la Upandaji miti Maekani wakiwa kwenye picha ya pamoja; wakati zoezi hilo likiendelea.

 

Mzumbe University,
P.O Box 1 Mzumbe,
Morogoro, Tanzania.
Tel: 255 (0) 23 2931220/1/2
Fax: 255 (0) 23 2931216
Cell: 255 (0) 754694029
Email: .
Go to top