Waratibu wa mradi wa Elimu ya juu kwa Mageuzi ya kiuchumi (HEET) wa Chuo Kikuu Mzumbe wamekutana katika kikao maalumu kwa ajili kujadili mpango wa utekelezaji wa kimkakati (USIP) ikiwa ni mwendelezo wa utekelezaji wa mradi huo wa miaka mitano wenye lengo la kuongeza udahili katika vyuo vikuu vya Umma nchini kwa kuboresha miundombinu ya kufundishia pamoja na kuwaandaa Wahitimu wenye ujuzi na uwezo wa kujiajiri na kuajiri kwa ajili kuchochea uchumi wa Taifa.
Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika katika Kampasi ya Chuo kikuu Mzumbe Dar es Salaam Upanga, Mratibu Mkuu wa mradi huo Prof. Eliza Mwakasangula amewahimiza Waratibu hao kuendelea kujituma kwa dhati na kusisitiza kuwa ushirikiano ndiyo nguzo muhimu katika kuleta ufanisi na kufanikisha malengo ya mradi na kuongeza kuwa kila mmoja anawajibu wa kuchangia mawazo na kujitolea kwenye utekelezaji wa mikakati iliyowekwa. "Ufanisi wa mradi wa HEET unategemea kazi yetu ya pamoja na kujituma kwa dhati," alisisitiza Prof. Mwakasangula.
Waratibu hao kwa pamoja walipitia na kujadili bajeti ya mwaka 2025/2026 ya mradi wa HEET kwa lengo la kuhakikisha kwamba rasilimali fedha za kutosha zinatengwa kuendana na malengo na vipaumbele vya mradi pamoja na kubainisha maeneo yaliyokuwa na changamoto katika utekelezaji kwenye bajeti iliyopita na kuyafanyia maboresho ili kuwezesha malengo ya mradi kutimia.
Naibu Mratibu wa mradi wa HEET chuo kikuu Mzumbe, Prof. Hawa Tundui akiongoza kikao hicho amesisitiza umuhimu wa kuboresha rasilimali za kujifunza na kufundishia kwa kuzingatia mahitaji halisi ya wanafunzi pamoja na kuanzisha mbinu mpya za ufundishaji, kuimarisha uhusiano na sekta binafsi na kuendelea kutoa huduma kwa jamii.
Aidha kikao hicho pia kilijadili njia za kutafuta rasilimali fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi midogo midogo inayoweza kuchangia maboresho makubwa kwenye huduma za elimu pamoja na kufanya uwekezaji kwenye teknolojia mpya na mafunzo kwa wahadhiri ili kuwapa ujuzi wa kisasa.
**************************
Kwa picha na matukio mengine, tembelea ukurasa wetu wa Facebook