Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha, ametembelea Shule ya Sekondari Kingo, na kufurahishwa na maendeleo ya Shule hiyo kitaaluma iliyopo  Manispaa ya Morogoro mkoani Morogoro. Prof. Mwegoha alitembelea shule hiyo na kukabidhi msaada wa Komputa Mbili kwa ajili ya kusaidia uandaaji wa mitihani na ufundishaji.

Akiwa ameambatana na Mkurugenzi wa Mipango, Mawasiliano na Wataalamu wa TEHAMA, Prof. Mwegoha alipata fursa ya kushiriki katika mjadala na viongozi wa Shule hiyo, na kupokea maelezo kuhusu utendaji na ufanisi wa shule hiyo kitaaluma, yenye wanafunzi 1145 na walimu 62.

Kutokana na ufanisi mzuri kitaaluma, ikiwa ni shule ya pili katika Manispaa kufanya vizuri katika matokeo ya kidato cha nne mwaka Jana, Prof. Mwegoha ameahidi chuo chake kuendelea kusaidia shule hiyo kutatua changamoto mbalimbali ambazo ziliainishwa na Mwalimu Mkuu, hususani Kuboresha matumizi ya TEHAMA na kuwajengea uwezo watendaji katika shule hiyo ili kuzalisha wanafunzi bora na wajuzi kwa kuendana na kasi kubwa ya mabadiliko ya kiteknolojia yanayoendelea ulimwenguni.

“Mzumbe tunaamini hawa ni wanafunzi wetu watarajiwa ndiyo maana tumefika kuwatembelea. Tunaamini kwa kuwajengea mazingira mazuri ya kujifunzia na kuwapa taaluma iliyo bora watakuwa wataalamu wazuri sana kwa Taifa letu” Alisisitiza Mwegoha

Mkuu wa Shule hiyo Mwl. Martine Kauki Joseph amesema, kwa sasa shule hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo ya uhaba wa vyumba vya madarasa na madawati (viti na meza), upungufu wa matundu ya choo 23 hasa kwa watoto wa kike, shule kukosa uzio na hivyo kusababisha utoro kwa wanafunzi pamoja na Maktaba.

Aidha, ameshukuru uongozi wa Chuo kwa kuwatembelea na kutoa msaada wa komputa ambazo zitasaidia sana kukabiliana na changamoto ya muda mrefu ya kukosa vitendea kazi, hasa uhifadhi wa taarifa na utungaji wa mitihani.

“Tumefarijika sana kuona Chuo Kikuu Mzumbe kimetufikia; tunatambua uwezo mkubwa wa chuo chetu katika kuandaa wataalamu bora hivyo tunaamini na sisi tutakuwa wanufaika wa utaalamu mlionao kwa wanafunzi wetu kujiunga na programu zinazotolewa Mzumbe, pamoja na mafunzo ya muda mfupi na mrefu kwa walimu wetu” alisisitiza

Kupitia mpango wake wa Huduma kwa Jamii, Chuo Kikuu Mzumbe, kimeendelea kutekeleza mpango wa kuwezesha wadau wake kutatua changamoto mbalimbali katika kuhakikisha Elimu inayotolewa katika ngazi mbalimbali inaboreshwa kuendana na mahitaji halisi ya kuboresha elimu nchini.

 

Ujumbe wa Chuo Kikuu Mzumbe, ulipowasili katika Shule ya Sekondari Kingo, na kupokelewa na wenyeji, uongozi wa Shule.

Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Kata, Mwl. Martine Kauki Joseph, akitoa taarifa kwa ujumbe wa Chuo Kikuu Mzumbe (hawapo pichani),

ofisini kwake, Kihonda mkoani Morogoro.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof. William Mwegoha (Mwenye Kaunda Suti) akimkabidhi Mkuu wa Shule ya Sekondari sehemu

ya vifaa vya Komputa vilivyotolewa na chuo hicho kama zawadi. Pembeni ni baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo wakishuhudia tukio la makabidhiano.

 

Mzumbe University,
P.O Box 1 Mzumbe,
Morogoro, Tanzania.
Tel: 255 (0) 23 2931220/1/2
Fax: 255 (0) 23 2931216
Cell: 255 (0) 754694029
Email: mu@mzumbe.ac.tz
Go to top