Chuo Kikuu Mzumbe ni Chuo Kikuu cha Umma nchini ambacho kilianzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Chuo Kikuu Mzumbe Na. 21 ya mwaka 2001. Sheria hiyo ilifutwa na Sheria ya Vyuo Vikuu Na. 7 ya mwaka 2005 ambayo ni sheria inayosimamia masuala yote yanayohusu Elimu ya Chuo Kikuu nchini Tanzania. Kwa sasa, Chuo kinatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Hati Idhini ya Chuo Kikuu Mzumbe, 2007 iliyotolewa chini ya Kifungu Na. 25 cha Sheria ya Vyuo Vikuu ya mwaka 2005.

Historia ya Chuo Kikuu Mzumbe ilianza kabla ya Uhuru wa Tanganyika ambapo mwaka 1953 Serikali ya Kikoloni ya Uingereza ilianzisha Kituo cha Mafunzo ya Serikali za Mitaa kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa machifu, maakida na watumishi wengine katika Serikali za Mitaa za wakati huo. Kituo hicho kilianzishwa katika eneo la Mzumbe lililoko Wilaya ya Mvomevo katika Mkoa wa Morogoro ambapo ndio Makao Makuu ya Chuo yalipo sasa. Baada ya Uhuru, Serikali iliendelea kupanua miundombinu na aina ya programu zilizokuwa zinazofundishwa katika Kituo hicho na mwaka 1963 kiliunganishwa na Kituo cha Mafunzo ya Mendeleo Vijijini Tengeru na kuitwa Kituo cha Mafunzo ya Serikali za Mitaa na Maendeleo Vijijini Mzumbe na kupanua uwigo wa fani za mbalimbali hususani katika maeneo ya utawala na menejimenti, sheria, ushirika, n.k. Mwaka 1972, Serikali ilikipandisha hadhi Kituo hicho na kuwa Chuo cha Uongozi wa Maendeleo Mzumbe (“Institute of Development Management Mzumbe, IDM Mzumbe”) kwa kuunganisha Taasisi ya Utawala wa Umma ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Kituo cha Mafunzo ya Serikali za Mitaa na Maendeleo Vijijini Mzumbe. Chuo cha Uongozi wa Maendeleo Mzumbe kilipewa jukumu la kutayarisha watendaji katika Taasisi za Umma. Kutokana na kukua kwa kwasi kwa IDM Mzumbe na kuongezeka kwa mahitaji ya viongozi wa kusimamia uendeshaji wa Taasisi za Umma, Serikali iliamua kukipandisha hadhi na kuwa Chuo Kikuu Mzumbe mwaka 2001. Chuo kimeendelea kukua kwa kasi kwa idadi ya wanafunzi na wafanyakazi na na kwa sasa, kina matawi tatu, yaani, Kampasi Kuu liyopo Morogoro, Ndaki ya Dar es Salaam na Ndaki ya Mbeya.

  READ MORE HERE

 

Mzumbe University,
P.O Box 1 Mzumbe,
Morogoro, Tanzania.
Tel: 255 (0) 23 2931220/1/2
Fax: 255 (0) 23 2931216
Cell: 255 (0) 754694029
Email: .
Go to top