Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia  Mhe.Prof.Joyce Ndalichako amevutiwa  na ubunifu wa mawazo na mbinu za Ujasiriamali unaofanywa na Wanafunzi  wa Chuo Kikuu Mzumbe wanaosoma shahada mbalimbali katika Chuo hicho na kusema kuwa anafurahishwa zaidi kuona Wanafunzi hao wanatumia vyema ujuzi na elimu wanayoipata kuwa Wabunifu zaidi katika kuzisogelea fursa za  kujikwamua kiuchumi.

Prof.Ndalichako ameyasema hayo wakati akifunga kilele cha Maadhimisho ya  kambi ya Ujasiriamali yanayoandaliwa kila mwaka  na Chuo Kikuu Mzumbe  Kampasi kuu Morogoro kwa lengo la kutoa mafunzo,kushindanisha, kuhasisha na kuendeleza ubunifu wa mawazo ya Ujasiriamali na biashara  ili kuwaandaa Wanafunzi wa fani mbalimbali  kuweza  kujiajiri na kushiriki katika ujenzi wa Tanzania ya viwanda pindi wanapohitimu masomo yao.

PICHA: Waziri Prof.Ndalichako akipokea maelezo ya bidhaa kutoka kwa Mwanafunzi  aliyeshiriki maadhimisho ya kambi ya Ujasiriamali Chuo Kikuu Mzumbe

“Nimefurahi  kuona ubunifu unaofanywa na vijana wetu na hii inatoa tafsiri sahihi kwa vitendo ya dhana ya  kujenga uchumi wa viwanda na inadhihirisha kuwa elimu mnayoipata imewasaidia na  kuweza kuchangamkia  fursa kwa kutatua changamoto zinazowazunguka katika mazingira yenu na hivyo mtaweza kujitegemea  baada ya kuhitimu.”

Waziri Prof.Ndalichako alisema  kupitia wizara yake atahakikisha kituo cha kuatamia ubunifu na biashara (Innovation and Business Incubation Center) cha Chuo Kikuu Mzumbe kinapatikana haraka kwa kutafuta rasilimali kwa Wadau wa maendeleo  ili kiweze kuwa chachu kwa vijana wote nchini wenye mawazo ya ubunifu,ujasiriamali na biashara kuweza kulelewa na kukuzwa kibiashara na kituo hicho na hivyo kuweza kujiajiri na kutengeneza Ajira.

PICHA: Waziri Prof.Ndalichako akipokea zawadi ya picha yake iliyochorwa na Mwanafunzi aliyeshiriki kambi ya Ujasiriamali.

Aidha Waziri Prof.Ndalichako alikitaka Chuo Kikuu Mzumbe kupitia kituo atamizi hicho kuhakikisha kinawezesha wabunifu wake wanashiriki katika mashindano ya kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU)  yanayoratibiwa na wizara yake kwa lengo la kuhamasisha ubunifu nchini,pia alizitaka Taasisi za Elimu ya juu nchini kuiga mfano wa Chuo Kikuu Mzumbe wa kuanzisha vituo atamizi na kutayarisha Wahitimu wenye mawazo ya kibunifu na mtazamo wa biashara na ujasiriamali.

Awali Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof.Lughano Kusiluka alisema kambi hiyo ya Ujasiriamali ilianzishwa mwaka 2017 kwa lengo la kuwashirikisha Wanafunzi wenye mawazo ya kibiashara na Ujasiriamali ambapo hukutanishwa na Wafanyabiashara waliobobea ili kujifunza na kupata uzoefu na kuwaandaa kutoka  chuoni hapo na biashara zao pindi wanapohitimu masomo yao.

PICHA: Waziri Prof.Ndalichako akitazama moja ya bidhaa maelezo ya  Mjasiriamali MWanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe

Aliongeza kuwa kambi hiyo ya Ujasiriamali ni maandalizi ya Chuo Kikuu Mzumbe kuanzisha kituo cha kuatamia ubunifu na biashara kwa ajili ya kuwawezesha vijana kupata utaalamu wa biashara na ujasiriamali kutoka kwa Wataalamu na wafanyabiashara wabobezi,kuwakutanisha na sekta husika ikiwemo kutatua changamoto ya mitaji kwa kuwaunganisha vijana na Taasisi za fedha zinazokopesha kwa riba nafuu.

Katika kambi hiyo  ya tatu Ujasiriamali ya Chuo Kikuu Mzumbe ,wanafunzi watatu kati ya sita waliotinga fainali walijinyakulia kitita cha shilingi Millioni moja kila mmoja baada ya mawazo yao ya ubunifu kushinda dhidi ya mawazo 48 yaliyoshindanishwa awali.

Mzumbe University,
P.O Box 1 Mzumbe,
Morogoro, Tanzania.
Tel: 255 (0) 23 2931220/1/2
Fax: 255 (0) 23 2931216
Cell: 255 (0) 754694029
Email: .
Go to top