Chuo Kikuu Mzumbe   kupitia mradi wake mpya wa ‘TESCEA’  kimeendesha warsha  ya kuwajengea uwezo wahadhiri katika mbinu bora za ufundishaji zinazosaidia wanafunzi kuweza kujiajirika  pindi wanapohitimu masomo yao ya elimu ya juu .

Akizungumza katika uzinduzi wa warsha hiyo inayoendelea katika  hoteli ya Morogoro, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof.Lughano Kusiluka  amesema  Chuo Kikuu Mzumbe ni mahiri katika kufundisha masomo ya biashara na menejimenti na sasa kinakwenda hatua ya mbele zaidi kwakuwaandaa wahitimu wa ndani na hata nchi nyingine  kutengeneza ajira  kabla ya kuhitimu masomo yao.

 

PICHA:Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof.Lughano Kusiluka,akizungumza na Wahadhiri wa Chuo Kikuu Mzumbe waliohudhuria warsha ya mabadiliko katika Sekta ya ajira kwa manufaa ya Jamii Afrika Mashariki (TESCEA) inayoendelea Morogoro.

Prof.Kusiluka ameeleza kuwa kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa waajiri dhidi ya  wahitimu  wa vyuo vikuu nchini na kuonekana   kutokuwa na  ujuzi wa kutosha na umahiri  katika fani walizosomea pindi wanapotaka kuajiriwa. Hivyo, Chuo Kikuu Mzumbe kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dodoma na vyuo vikuu  viwili kutoka Uganda (Uganda Martys na Gulu),  pamoja na   asasi za AFELT, LIWA, ASHOKA  kutoka Kenya na INASP kutoka Uingereza,  wameanza kwa kuwajengea  wahadhiri ili kubadili mbinu za ufundishaji zitakazowawezesha wahitimu kuwa na maarifa, ubunifu na ujuzi zaidi  kutambua na kutumia fursa zilizopo  ili kutengeneza ajira au kuajiriwa.   

Kwa upande  wake mwezeshaji wa warsha wa asasi ya umoja wa Vyuo vikuu vinavyofundisha  mbinu  zinazohitajika katika kuboresha ufundishaji Afrika Mashariki (AFELT) na Mhadhiri wa  Chuo Kikuu cha Daystar cha Kenya Prof. Charles Kingsburry,  amesema ni muhimu sasa kubadili mfumo wa ufundishaji unaowafanya wahitimu kujua vitu kulingana na elimu wanayofundishwa darasani pekee na kwa kutegemea mitandao ya intaneti na badala yake mbinu mpya za ufundishaji ziwajenge  katika ubunifu ,maarifa,mbinu na stadi halisia zitakazowawezesha kujiajiri wao na kuweza kuajiri watu wengine. Hii ina lengo si   tu la kuwafanya wahitimu kujua vitu tofauti bali kuwajenga kuwa watu tofauti wanaoleta mabadiliko chanya kwa jamii nzima na kujinufaisha wao na  jamii zinawazunguka kupitia elimu waliyopata.

Naye mwezeshaji  mwingine toka Asasi ya AFELT na mhadhiri wa Chuo Kikuu, Afrika Nazarene cha nchini Kenya Dkt. Kendi Muchungi amesema wahitimu wa Vyuo Vikuu vyote vya Afrika Mashariki hawatofautiani na wamekuwa wakikosa uwezo wa kujiajiri na  kuajiriwa na hivyo kushindwa  kuisaidia jamii katika suala la ajira kupitia elimu waliyopata,badala yake wamekuwa wakitegemea kuajiriwa.   Hivyo ni  imani yake kuwa mpango huo utaleta mabadiliko  kwa wahadhiri wa vyuo vikuu katika ufundishaji na  kunufaisha jamii nzima ya Afrika Mashariki kupitia wasomi wachache.  

Wakati huo huo mratibu  wa Mradi wa ‘TESCEA’  kutoka Chuo Kikuu Mzumbe,Dkt.Albogast Musabila amesema pamoja na  lengo  kuu la  mpango wa mradi huo la kuwajengea wahitimu uwezo wa kujiajiri na kuajiri,Chuo Kikuu Mzumbe  kwa ushirikiano na wadau wa Sekta ya ajira, wahadhiri na wanafunzi kimeanza mchakato wa kukusanya maoni ya wadau kwa ajili ya  kuandaa mapendekezo  yatakayozingatiwa wakati wa kuboresha mitaala na kuanzisha mitaala mipya.

Mzumbe University,
P.O Box 1 Mzumbe,
Morogoro, Tanzania.
Tel: 255 (0) 23 2931220/1/2
Fax: 255 (0) 23 2931216
Cell: 255 (0) 754694029
Email: .
Go to top